Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vinatoa taarifa potofu kuhusu mchakato wa Mwenyekiti wa sasa wa CCM Dkt. Jakaya Kikwete kukabidhi kijiti cha uongozi wa CCM kwa Rais John Pombe Magufuli kama ilivyo mila na desturi ya Chama Cha Mapinduzi.
Yamekuwepo madai eti Mwenyekiti amekataa au anachelewesha kukabidhi kijiti.
Habari hiyo sio kweli kabisa na ni kinyume chake, kwani Dkt. Kikwete amekuwa akisisitiza kukabidhi madaraka mapema iwezekanavyo. Kwa ajili hiyo kwenye kikao cha Mei 3, 2016 alikataa kusiongezwe agenda nyingine ambazo zitalazimisha Mkutano Mkuu Maalum kuchelewa kufanyika kwa sababu ya kukamilisha maandalizi ya agenda hizo. Alisisitiza agenda iwe moja tu.
Dhamira ya kufanyika Mkutano Mkuu maalum mwezi Juni, 2016 iko pale pale. Kilichoelezwa kwenye kikao ni kutaka kukamilisha utaratibu wa kupata fedha za kugharamia mkutano huo. Taratibu zikikamilika tarehe itapangwa. Mipango ya kutafuta pesa inaendelea na ikikamilika tarehe itatangazwa.
Tunawataka wana-CCM wasihamanike wala kubabaishwa na taarifa za upotoshaji zinazofanywa na watu wenye nia mbaya na CCM. Hawa ni wale wale ambao wamekuwa wakiiombea mabaya CCM bila ya mafanikio.
Pia tunapenda kukanusha madai ati kuwa Mwenyekiti Kikwete aliwatahadharisha Wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu ukimya wa Ndugu Edward Lowassa. Hakuna wakati wowote kauli kama hiyo aliitoa. Ni uzushi mtupu. Jina la Ndugu Lowassa halikutajwa kabisa.
Aidha, tunapenda kukanusha madai ya kufanyika mkutano baina ya Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais na Katibu Mkuu wa CCM kuhusu uchaguzi wa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM. Hapajawahi kufanyika mkutano wa aina hiyo siku yoyote na mahali popote. Hivyo madai ya kuwepo kwa tofauti baina ya Viongozi wakuu kuhusu nani achaguliwe kuwa Katibu wa Wabunge wa CCM hayana msingi wowote.
Kamati Kuu iliteua Wabunge wanne kugombea na kuwaachia Wabunge wa CCM kuamua. Kuhusisha Viongozi na hasa kuzua kuwepo kutokuelewana ni jambo la kusikitisha. Ni taarifa ya uongo yenye nia ovu kwa CCM na Viongozi wake.
Tunapenda kuwatahadharisha waandishi wa habari kuandika habari za ukweli. Waache kuzua mambo yenye kupandikiza chuki na mgawanyiko usiostahili kuwepo ndani ya CCM na kuyaeneza kwa watu. Waheshimu maadili ya kazi zao.
Napenda kuwahakikishia na kusisitiza kuwa hakuna mgogoro wa kukabidhi kijiti cha uenyekiti katika CCM na wala hautakuwepo.
Imetolewa na;
Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
05/05/2016
No comments:
Post a Comment