Thursday, May 5, 2016

dangote atanjwa kuwa chanzo cha kutumbuliwa kairuki

Wakati aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ametajwa kutenguliwa uteuzi wake kwa kukataa kuchukua mshahara wa Serikali kwa miaka mitatu mfululizo, uchunguzi umebaini kuwa jipu la kusamehe kodi Kampuni ya Saruji ya Dangote ndilo lililomwondoa.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa mbali na Juliet Kairuki kutochukua mshahara wa Sh 5,000,000 kila mwezi aliopangiwa na Serikali kwa miaka mitatu, kwa maana kuwa ameacha kuchukua wastani wa Sh milioni 180 kwa muda huo, anatuhumiwa kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wawakezaji bila kufuata utaratibu au sheria za nchi.

“Hili la mshahara ni cha mtoto. Amewadanganya wawekezaji wengi kuwa anaweza kuwapa msamaha wa kodi ya VAT, na sasa Serikali hii ilipoingia madarakani ikasema hana mamlaka hayo. Mwekezaji wa kwanza aliyedanganywa ni Dangote,” anasema mtoa taarifa wetu.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa Novemba, 2015 Kampuni ya Dangote iliingiza nchini makaa ya mawe tani 35,000 kutoka Afrika Kusini na kutaka makaa haya yasamehewe kodi zote.

“Kwa kweli tulishangaa sana. Kwanza, makaa ya mawe si bidhaa za mtaji (capital) bali ni za matumizi tu (consumables). Vifaa vinavyosamehewa kodi ni zile zinazotumika kuzalisha bidhaa nyingine leo, kesho, mwakani au miaka mitano ijayo na kuendelea, ila makaa ya mawe ukiyachoma yanaisha siku hiyo hiyo, hivyo hii si mtaji.

“Ukiacha hilo, hawa watu wa Dangote wameambiwa wanunue makaa ya mawe kutoka Kiwira au Ngaka, lakini hawataki,” kinasema chanzo chetu na kuongeza kuwa kwa mwaka uliopita, waliagiza tani 2,000 tu za makaa ya mawe kutoka Tancoal kinyume cha makubaliano ya kuongeza ajira nchini.

Afisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amefichua katika uchunguzi huu kuwa kinachoendelea kwenye Kampuni ya Dangote ni balaa. “Hii kampuni tulidhani imekuja hapa kukomboa wananchi, lakini uhalisia siyo.

“Kampuni hii inafanya malipo bila kutoa kodi ya zuio, bidhaa inazoingiza nchini pamoja na nyingine kupata misamaha ya kodi bado inaongeza bei zinakuwa ghali mno kwa maana ya kuongeza gharama za uzalishaji na hivyo kupunguza kiasi cha kodi kinachostahili kulipwa… ni shida,” anasema afisa huyo kwa uchungu.

Kutokana na mkanganyiko huo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, ameunda timu ya kufanya ukaguzi maalumu kwa Kampuni ya Dangote ambayo imewakuta na hatia.

“Hiyo bilioni 20 ni uchunguzi wa awali, tunaweza kupata kiasi kikubwa zaidi. Tunawashukuru kwa kuandika habari za ukwepaji kodi, na nakuhakikishia sisi tunafuatilia kila mnachochapisha,” anasema mtoa habari wetu.

Afisa mwingine wa TRA anasema mbinu kubwa inayotumiwa na Dangote na kampuni nyingine ambazo tayari TRA imekwishaibaini mbinu wanazotumia kupunguza faida (Tax Base Erosion), kwa kuingia mikataba yenye gharama kubwa na kampuni walizo na uhusiano nazo kibiashara, kuonesha wametumia gharama kubwa wakati uhalisia wanafanya mbinu za kukwepa kodi.

Akizungumzia sakata hili, Mejena Mkuu Mwandamizi wa Kampuni ya Dangote, Vidya Dixit, amekiri kupokea ankara ya malipo kutoka TRA yenye thamani ya bilioni 20 na akasema: “Wakaguzi wa TRA wako hapa, wamefanya uchunguzi wao, wametuletea madai yao, na sisi tunawasiliana na mshauri wetu wa masuala ya kodi, ikithibitika kuwa tunadaiwa kiasi hicho Dangote ni kampuni kubwa, tutalipa.”

Dixit amesema TRA wamekagua mikataba mbalimbali wanayotumia akina Dangote kuagiza bidhaa na huduma, na wakaja na kiasi hicho, hivyo kwake halioni kama ni tatizo, washauri wao wa masuala ya kodi wakikuta ni kweli watalipa tu. Chanzo chetu kimetueleza kuwa mshauri wao ni Kampuni ya PriceWaterhouseCoopers (PWC) ya Afrika Kusini.

Meneja huyo alijibu pia swali kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TRA) inawadai dola 2,867,400 za Marekani (sawa na Sh bilioni 6.3), kwa kusema: “Mimi sisimamii idara ya uhasibu. Madeni hayo yanaweza kuwapo, ila Dangote ni kampuni kubwa, kama kuna madeni ya aina yoyote tutalipa tu baada ya kujiridhisha kuwa ni madeni halali.”

Kuhusu suala la tani 35,000 za makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini, alisema wao kama Dangote hawapaswi kulaumiwa kwani walifuata taratibu zote: “TIC walitupa sisi msamaha wa kodi, sasa tumezungumza na Waziri wa Fedha akasema TIC hawana mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi bila kutangaza kwenye Gazeti la Serikali (GN) na kweli hakukuwapo GN yoyote.

“Sasa hapa tunapata tabu kidogo, idara moja ya Serikali inasema hivi na idara nyingine inasema vile, tunapata shida kidogo,” anasema Dixit. Katika makaa hayo ya mawe pekee ambayo wanatakiwa kuyanunua kutoka nchini, Dangote wanadaiwa wastani wa Sh bilioni 1.1.

Kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwa kiwanda hicho kuwa kimewageuka wafanyabiashara wadogo na kupendelea wafanyabiashara wakubwa kwa njia ya kuwauzia saruji nyingi na kutowajali wadogo, Dixit anasema wao hawana ubaguzi na ucheleweshaji unaweza kutokea kunapotokea dharura.

Anasema kuna wakati wanaangalia nani ana ghala kubwa la kuhifadhia saruji kiasi gani, ila hiyo haiondoi ukweli kwamba hawabagui yeyote anayetaka kununua na kuuza saruji ya Dangote.

“Ukisema kuna walioshindwa kupata saruji kwa wiki moja au mbili, hilo naweza kukuelewa, lakini miezi miwili, wala asikudanganye mtu. Hilo haliwezekani. Ni kweli kule Lindi tunakotoa chokaa, machimbo yote kwa siku tatu zilizopita yalijaa maji, tukashindwa kupata chokaa, lakini zaidi ya hapo kila mtu anapewa fursa sawa ya kununua saruji bila ubaguzi,” anasema Dixit.

Awali, baadhi ya wafanyabiashara waliilalamikia Kampuni ya Dangote kuwa inauza saruji kwa upendeleo, hali inayowafanya wakose mapato kwani wamekopa mikopo benki na wanaishia kutopata saruji kwa wakati hivyo wanashindwa kulipa hiyo mikopo.

“Kuna mfanyabiashara ameweka kwenye akaunti ya Dangote Sh bilioni 2.5, huyu ndiye anayepewa saruji sisi wengine tunapuuzwa. Watanzania wengi wamekopa benki wastani wa Sh milioni 20, 30 au 50 wanaziweka kwenye kampuni ya Dangote na hawapati hiyo saruji. Hii inatutia hasara mno. Tunataka usawa katika biashara hii,” anasema mmoja wa wafanyabiashara anayedai ameweka Sh milioni 25 kwenye Kampuni ya Dangote, lakini hapatiwi saruji.

Pia, wanalalamikia bei kubwa ya saruji ya Dangote kwani wakati kiwanda kinaanza kujengwa Watanzania walitangaziwa kuwa mfuko mmoja wa saruji ungeuzwa kwa Sh 8,000, lakini sasa bei inafikia Sh 16,000 kwa mikoa kama Mwanza na kwa Dar es Salaam inauzwa kati ya Sh 10,800 na 12,500.

Kamishna Mkuu wa TRA, Kidata, hakuwa tayari kulizungumzia kwa undani suala la Dangote zaidi ya kusema: “Hili suala lipo, tunalifanyia kazi, ni mapema mno kulizungumzia kwa sasa.”

Hata hivyo, afisa mwingine mwandamizi alishangaa kusikia kuwa Dangote bado wanatafuta ushauri wa kisheria kama walipe kodi hiyo au la: “Hawa waliishakwenda hadi kwa Bwana Mkubwa wakakubali kulipa, sasa leo inakuwaje wanatafuta ushauri?” Alihoji afisa huyo.

Alichosema ni kuwa kila mfanyabiashara mkubwa kwa mdogo ajiandae kulipa kodi. “TRA haitaingilia mapato halali ya mfanyabiashara yeyote, ila kwa yeyote anayekwepa kodi hili halitavumiliki. Serikali ya sasa inasema hapa ni kazi tu, hakuna habari ya jina kubwa au dogo. Jipu ni jipu tu, bila kujali ni kubwa au dogo, yote yatakamuliwa tu.”

Source: Jamhuri

No comments:

Post a Comment